Monday, 30 December 2013

Bebe Cool alipwa fidia ya zaidi ya milioni 257 za Tanzania kufuatia kesi ya kupigwa risasi na polisi.

Awali Bebe Cool alifungua mashitaka akidai zaidi ya milioni 533 za Tanzania, kufuatia kujeruhiwa sehemu ya mguu wake.
Bebe Cool alidai kiasi hicho cha pesa kama fidia ya kipato alichopoteza katika kipindi cha miezi 9 hadi 12 wakati akiuguza majeraha ya risasi.
Msanii huyo aliiambia mahakama kuu ya Uganda kuwa alikuwa amepata dili ya kufanya matangazo na MTN na Century Bottling Co Ltd, makampuni ambayo yangemlipa kiasi kikubwa cha pesa. Na kuongeza kuwa alikuwa katika maandalizi ya kurekodi nyimbo 16 kwa ajili ya album yake ambayo ingemuingizia mkwanja mrefu.
Hata hivyo, Bebe Cool alishindwa kuwasilisha vielelezo mahakamani kuonesha hasara hiyo, hivyo mahakama ikaamua alipwe milioni 257 badala ya milioni 533 alizodai.
Bebe Cool alipigwa risasi January 29 mwaka 2010 na polisi anayejulikana kwa jina la Anthony Achikan muda mfupi baada ya kupiga show kwenye jukwaa moja na R.Kelly jijini Kampala.
Bebe Cool na kundi lake walikuwa barabarani na magari yao mida ya saa tisa usiku wakielekea Nakumatt, ambapo walikutana na polisi aliyewasimamisha.
Yalitokea majibishano ya muda mrefu kati ya Polisi huyo na Bebe Cool, ndipo polisi huyo alifyatua risasi zilizomjeruhi mwimbaji huyo.
Polisi huyo alikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya usalama ambapo alifunguliwa mashitaka kwa kufanya jaribio la kuua.
Polisi huyo alikutwa na hatia na hadi sasa anaendelea kutumikia kifungo cha miaka 9 jela.

0 comments:

Post a Comment