
Utata
umeibuka kuhusu alipo mfanyabiashara maarufu nchini, Alex Masawe baada
ya kuwepo kwa tetesi kuwa ameachiwa huru huko Dubai, Falme za Kiarabu
(UAE) alikokuwa akishikiliwa.
Masawe
ambaye alikamatwa katika uwanja wa ndege huko UAE akitokea Afrika
Kusini, kati ya Juni 20 na 25, mwaka jana, anatuhumiwa kwa makosa
mbalimbali yakiwamo ya mauaji.
Mkuu
wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) - Tanzania, Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP), Gustav Babile alikiri kuwapo kwa taarifa
kwamba Masawe ameachiwa huru na hayupo Dubai ingawa bado tawi la
Interpol katika nchi hiyo halijatoa taarifa yoyote.
“Tumejaribu
kuwasiliana nao mara kwa mara kuhusu kumrudisha nchini lakini
hawajajibu lolote. Hivi karibuni tuliwasiliana nao lakini hawajatujibu,
kwa hiyo tumebaki na maswali. Kwa kifupi hatujui alipo hadi sasa,”
alisema Kamishna Babile.
Alisema
awali, baada ya kukamatwa huko Dubai, Tawi la Interpol Tanzania
lilikuwa linafanya mchakato wa kumrudisha nchini ikiwamo kutuma ombi la
kumrejesha mhalifu nchini, lakini ghafla mawasiliano yakakatika.
“Taarifa zilizopo ni kuwa Masawe ameachiwa huru, kwa vigezo gani hatuelewei,” alisema Babile.
Babile
alisema iwapo atakuwa ameachiwa na polisi wa UAE, basi itakuwa
ameachiwa kutokana na sheria za nchi hiyo ingawa bado Tanzania
itaendelea kumsaka kwa udi na uvumba.
“Sisi
tutaendelea kumsaka kama kawaida, iwapo atakamatwa nchi nyingine au
ikitokea akaonekana hapa nchini, tutaendelea na mchakato wa kumfungulia
kesi kwa sababu sisi tunajua kuwa ana makosa,” alisema Babile.
Massawe
alitajwa mahakamani Aprili 4, mwaka jana katika kesi ya mauaji ya
mfanyabiashara, Onesphory Kituly ambaye aliuawa katika mazingira ya
kutatanisha Novemba 6, 2011 nyumbani kwake Magomeni, Dar es Salaam.
Katika
kesi hiyo, mshtakiwa wa kwanza ni mfanyabiashara Abubakar Marijani,
maarufu kama ‘Papaa Msofe’ na mshtakiwa mwingine ni Makongoro Joseph
Nyerere.
Nyerere
aliwahi kulalamika mbele ya Hakimu Mkazi, Agnes Mchome anayesikiliza
kesi hiyo, akidai kwamba kumekuwa na ucheleweshaji wa shauri hilo
kutokana na ndugu wa marehemu Kituly kutaka Massawe akamatwe ili
ajumuishwe.
Mtuhumiwa
huyo aliomba jalada la kesi yao lipelekwe mahakamani hapo kwa ajili ya
kulifanyia kazi. Alitoa malalamiko hayo baada ya Wakili wa Serikali,
Mwanaisha Kombo kudai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na
kuomba tarehe mpya ya kutajwa kwake.
Wednesday, 15 January 2014
MFANYABIASHARA ALEX MASAWE ADAIWA KUWA YUPO HURU.
12:36
No comments
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment